Wizara ya Fedha na Mipango imependekeza kupunguzwa kwa adhabu zinazotolewa chini ya Sheria ya Usalama Barabarani (SURA) namba 168 kwa makosa ya pikipiki na bajaji kutoka shilingi elfu 30 za sasa hadi shilingi elfu 10 kwa kosa moja.

Waziri wa wizara hiyo Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuweka adhabu kwa kuzingatia uwezo wa kulipa.

Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo jana  Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Amesema adhabu kwa makosa mengine ya vyombo vya moto zinazotolewa kwa mujibu wa sheria zinaendelea kubaki kama ilivyo sasa.

Amesema Serikali inapendekeza kupunguzwa adhabu kwa makosa ya pikipiki na bajaiji baada ya kubaini kuwa madereva wa vyombo hivyo ambao wengi wao ni vijana, wamekuwa wakipata usumbufu wa kulipa faini kutoka kwenye vipato vyao pale panapotokea uvunjaji wa Sheria ya Usalama Barabarani hata unaofanywa na abiria wao.