Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ataendelea kuwasalimia watu anapokuwa ziarani licha ya kitisho cha usalama, baada ya hapo jana kuzabwa kofi na mtu mmoja kusini mwa Ufaransa. 

Msemaji wa serikali Gabriel Attal amesema hii leo ni wazi kwamba Macron ataendelea na ziara zake na ataendelea kuwasalimia watu. Amesema litakuwa ni jambo la kushangaza sana iwapo rais hatawasalimia watu kutokana na mtu mmoja aliyetaka kumshambulia. 

Mshambuliaji huyo wa Macron mwenye miaka 28, Damien T, bado anashilikiwa mahabusu na anatarajiwa kufunguliwa mashitaka ya kumshambulia kiongozi wa umma, na anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitatu jela. 

Kisa hicho kimeibua mjadala mkubwa kuhusu iwapo rais huyo yuko salama kuendelea na ziara zake na kusalimiana na makundi ya watu.