Aliyekuwa afisa wa polisi Derek Chauvin amehukumiwa kifungo cha miaka 22 na nusu jela baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd, mauaji ambayo yalisababisha maandamano makubwa zaidi ya kukomesha ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi.

Chauvin ambaye ni mzungu mwenye umri wa miaka 45, alitoa rambi rambi  zake kwa familia ya Floyd katika mahakama ya Minneapolis bila ya kuomba msamaha, kabla ya jaji Peter Cahill kutoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 22 jela, adhabu ambayo ni ndogo tofauti na kifungo cha miaka 30 walichokuwa wanataka upande wa mashtaka.

 "Kifungo hiki kimetokana na utumiaji mbaya wa nafasi yako kama afisa wa polisi na mamlaka, na pia ukatili uliomfanyia George Floyd," jaji Cahill alimwambia Chauvin aliyekuwa akisikika kwa makini hukumu hiyo.

Uamuzi huo ulisomwa mwisho wa kikao cha kesi hiyo ambapo korti iliutazama ujumbe uliorekodiwa na binti wa Floyd, Gianna Floyd, mwenye umri wa miaka saba.

Wakili wa familia ya Floyd ameutaja uamuzi huo kuwa hatua ya kihistoria kuelekea kupatikana kwa maridhiano na usawa wa jamii mbalimbali.