Na Shamimu Nyaki, Dar es Salaam
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Mei 21,2021 wakati akizindua Kongamano la kuenzi mchango wa Tanzania kwenye ukombozi wa Afrika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam ya kuitaka Wizara ikae na Wizara ya Utumishi na TAMISEMI kutatua changamoto za kimuundo kwenye Sekta za Utamaduni na Michezo.

Katibu Mkuu wa Habari Dkt. Hassan Abbasi ameongoza kikao hicho kilichoshirikisha Makatibu Wakuu wa Wizara za TAMISEMI na Utumishi, kwenye kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo nchi nzima ambapo amesema maelekezo yote yamefanyiwa kazi na kukamilika kilichobaki  ni kuandaa nyaraka ili fanikisha  utekelezaji wa maelekezo hayo.

"Kikao hiki kimejadili na kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa aliyotoa Mei 21,2021 wakati akifungua Kongamano la Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo kufanya marekebisho ya Muundo wa kada za Maafisa Utamaduni na Michezo, na tayari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora tumeyafanyia kazi" amesema Dkt.Abbasi.

 Amesema Muundo kama huo unatengenezwa kwenye Sekta ya Sanaa ili taaluma za Sekta hizo zitumike kwa ufanisi.

Aidha Dkt. Abbasi amesema kuwa Sera ya Michezo haina changamoto yoyote na inaendelea kutekelezwa kwa namna inavyoelekeza ikiwemo kuwa na miundombinu ya michezo, kutambua michezo kama taaluma, kuwa na vituo vya kukuza vipaji na mambo mengine yaliyoanishwa katika Sera hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Utumishi, Dkt. Francis Michael amefafanua kuwa muundo wa sasa umeboreshwa ambapo mtaalam mwenye fani nyingine ambazo siyo za michezo lakini ana uzoefu kwenye michezo na amepata mafunzo ya michezo anakuwa na nafasi ya kuwa kwenye kada Afisa Michezo.

Dkt.Michael amesema muundo wa awali ulikuwa unashindwa kuitambua kada ya maafisa michezo hivyo kuwafanya wataalam  kushindwa kufanya majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anaeshughulikia Elimu Gerald Mweli amesema kuwa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo kitatengewa bajeti kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya sekta hizo ambapo amesisitiza maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha ili waweze kupimwa utendaji wao kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma

Naye, Afisa Utamaduni wa Tabora Tito Lulandala kwa niaba ya maafisa Utamaduni na Michezo ameishukuru Serikali kwa namna ilivyotatua changamoto za Maafisa hao hatua ambayo itaboresha utendaji kazi wao.