Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imeunda jopo la ngazi ya juu la wataalamu kwa ajili ya ugharamiaji wa Kilimo (AGRICULTURE FINANCING) ambapo timu hiyo itaongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe (Mb).
Timu hiyo itajumuisha watendaji wakuu wa mabenki na taasisi za fedha ambapo itakuwa na wajumbe ambao ni Mkurugenzi Mtendaji CRDB, Mkurugenzi Mtendaji NMB, Mkurugenzi Mtendaji TADB, Mkurugenzi Mtendaji NBC, Mkurugenzi Mtendaji PASS Trust, Mkurugenzi Mtendaji TPB, Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Azania, Mkurugenzi Mtendaji TIB-DFI na Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ametangaza timu hiyo tarehe 13 Mei 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma huku Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo akitajwa kuongoza sektretarieti pamoja na kuwa mjumbe wa jopo hilo.
Amesema kuwa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2018 inaonesha kuwa kiwango cha utoaji mikopo (lending share) kwenye sekta ya kilimo kilikuwa kinashuka kutoka asilimia 12 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2018.
Pia, Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2019 inaonesha kuwa mtaji uliowekezwa katika sekta ya kilimo kutoka katika Benki za Biashara hapa nchini ulikuwa shilingi Trilioni 1.8 sawa na asilimia 9.2 ya mikopo yote kwa mwaka. Kiwango hicho kwa sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 58 ya watanzania ni kidogo ikinganishwa na asilimia 10.5 na asilimia 17.1 katika sekta za uzalishaji viwandani na biashara mtawalia.
Waziri Mkenda amesema kuwa kutokana na hali hiyo tarehe 22 Aprili, 2021 aliwaita wakuu wa taasisi za fedha hususani mabenki ya biashara na kujadiliana nao hitaji la kuwa na mfumo wa uhakika wa kugharamia sekta ya kilimo.
Amebainisha kuwa malengo ya kikao hicho yalikuwa ni kujadiliana kuhusu namna bora ya kufanya mapinduzi katika kilimo kwa kuhakikisha mitaji inapatikana kwa wakulima na wadau katika kilimo itakayowawezesha kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa mazao mbalimbali ya kilimo ikiwemo kupata pembejeo, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na uhakika wa kupata masoko ya mazao wanayozalisha.
AMesema kuwa Uwekezaji katika sekta ya kilimo umekuwa mdogo ikilinganishwa na sekta nyingine za uchumi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji ya uhakika, ardhi, vivutio vya uwekezaji na ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao na bidhaa za kilimo.
Kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), sekta ya kilimo imekuwa ikipata uwekezaji mdogo ikilinganishwa na sekta nyingine kama Viwanda, Biashara, Huduma, Mawasiliano na Ujenzi. Kiasi cha uwekezaji kwa kipindi cha mwaka 1997 hadi 2018: Kilimo na mifugo (14.18%), viwanda (18.01%), Mawasiliano (15.54%), miundombinu (12.62%).
Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2018 inaonesha kuwa kiwango cha utoaji mikopo (lending share) kwenye sekta ya kilimo kilikuwa kinashuka kutoka asilimia 12 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2018. Pia, Taarifa ya Kadhalika, Waziri Mkenda ameitaja hali ya Uchumi ya mwaka 2019 inaonesha kuwa mtaji uliowekezwa katika sekta ya kilimo kutoka katika Benki za Biashara hapa nchini ulikuwa shilingi Trilioni 1.8 sawa na asilimia 9.2 ya mikopo yote kwa mwaka.
Amesema Kiwango hicho kwa sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 58 ya watanzania ni kidogo ilikinganishwa na asilimia 10.5 na asilimia 17.1 katika sekta za uzalishaji viwandani na biashara mtawalia.
Amesema, ili kufanikiwa katika sekta ya kilimo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejiwekea Vipaumbele ambavyo ni pamoja na Utafiti hususani wa mbegu bora na mbinu bora za kilimo; kuimarisha huduma za ugani ili kuongeza tija ambayo ni jawabu la kuzalisha mazao kwa wingi na yenye ubora ndani ya eneo dogo; Kuongeza uzalishaji wa mbegu, Masoko, Umwagiliaji na Ugharamiaji wa kilimo (Agriculture financing).
Waziri Mkenda amesema kuwa Vipaumbele hivyo vyote ni dhahiri kwamba vinahitaji msukumo na uwekezaji mkubwa ili kuweza kufikia malengo ambayo Wizara imejiwekea.
MWISHO