Na Eliud Rwechungura.
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amekutana na kufanya kikao na wadau mbalimbali wa usafirishaji, uingizaji na utoaji wa mizigo bandarini.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kililenga kujadili kwa pamoja changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wadau hao ambazo zimekuwa zikiathiri mazingira na hali ya biashara hapa nchini.

“Serikali haifanyi biashara, hivyo haiwezi kukuza biashara bila mchango wa sekta binafsi na bandari ndio mlango mkuu wa uchumi wa nchi na hauwezi kusema unaboresha mazingira ya biashara kama hujagusa kuiboresha bandari”

“Tunaamini kwamba, tukiweka mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa wafanyabiashara wetu, biashara zitakua na biashara zikikua, uchumi wa nchi unakua na uchumi ukikua mapato ya nchi yanaongezeka zaidi” amesema Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo

Aidha, kikao hicho kilitumika kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau hao kuhusu utendaji wa majukumu yanayofanywa na Shirika la Viwango Tanzania TBS katika Bandari ya Dar es Salaam, hususan jukumu jipya la ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Angelina Ngalula amelalamikia utaratibu na utoaji wa huduma wa Shirika la Wakala wa Meli nchini (TASAC) pindi wanapowahudumia wateja wao huku akiomba kuwekwa kwa utaratibu mzuri ambayo utawasidia kufanyabiashara kufanya biashara bila vikwazo mabimbali vilivyopo sasa katika eneo la bandari kwani ndio moyo wa uchumi wa nchi

Kikao hicho kimefanyika Leo Mei 03, 2021katika ukumbi wa Mikutano wa Bandari ya Dar es salaam na kimehudhuriwa na wadau mbalimbali na wawakirishi wa Taasisi za TAFFA- Tanzania freight forwarding Association, TATOA- Tanzania Truck Owners Association, TASAA- Tanzania Shipping agency’s Association, CIDAT- Container Inland Deports Associations of Tanzania, TSC- Tanzania Shippers Council, TICTS- Tanzania International Container Terminal Services.