Waziri Ummy Ameagiza Kusimamishwa Kazi Kwa Wakuu Wa Idara Wanne Kupisha Uchunguzi
Angela Msimbira, SHINYANGA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza kusimamishwa kazi wakuu wa Idara Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kushindwa kusimamia kwa weledi ukamilishaji wa ujenzi wa Machinjio ya kisasa iliyopo Ndembezi mjini Shinyanga ili kupisha uchunguzi kwa tuhuma zinazowakabili.
Akikagua mradi huo jana katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga Waziri Ummy amesema kuwa amewasimamisha kazi wakuu hao wa idara kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa kumshauri Mkurugenzi kuhusu mradi huo na kushindwa kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
Amewataja waliosimamishwa kupisha uchunguzi kuwa ni aliyekuwa Kaimu Afisa Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji Bw. Gwakisa Mwaisyeba, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Dkt Tito Kagize, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Kassim Thadeo na Mkuu wa Kitengo cha manunuzi Bw.Godfrey Mwangailo na amemuagiza Mkuu wa Mkoa Bw.Dkt Philemon Sengati kuhakikisha anaunda tume itakayochunguza ubadhilifu wa fedha ambao umesababisha kusuasua kwa ujenzi wa Machinjio hiyo.
Waziri Ummy amesema kutokamilika kwa Mradi wa Machinjio ni aibu kwa watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na inarudisha nyuma maendeleo ya Manispaa hiyo.
‘Ukamilishaji wa machinjio hii kutasaidia kuongeza mapato ya wananchi na Halmashauri kwa ujumla kwa kuwa Halmashauri ikikusanya mapato itaweza kutatua changamoto katika Sekta ya Afya, Elimu na miundombinu ya barabara’ alisema
Mbali na kuwasimamisha Wakuu hao wa Idara pia ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuwaandikia barua Mkandarasi wa mradi huo , Kampuni ya Home Africa pamoja na Mhandisi mshauri B.J Amour nao wapelekwe bodi ya Mkandarasi ili iwawajibishe.
“ Mradi huu haukusimamiwa vizuri na tunawatesa watu wa shinyanga mpaka leo haujakamilika na fedha hazionekani, kuna shilingi milioni 800 zimelipwa kwa wakandarasi bila kuhakikiwa wala kujiridhisha. Huu mradi ni aibu kwa Shinyanga kwa hiyo nawasimamisha kazi kwa wiki mbili ili wapishe uchunguzi” amesema Waziri Ummy
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema kuwa mradi huo ulitengewa kiasi cha shilingi bilioni 5.7 lakini hadi sasa zimetumika kiasi cha shilingi bilioni 5.1 na shilingi milioni 600 hazijulikani zilipo wakati mradi haujakamilika, amesisitiza kuwa katika ripoti ya mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ilieleza kuna ufisadi na mradi haukukamilika vizuri.
Hatua hiyo ya Waziri Ummy imekuja baada ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. David Nkulila kueleza kuwa kamati ya fedha ya halmashauri hiyo kupitia baraza la madiwani walikuwa wameanza kuchukua hatua baada ya kubaini kuwa thamani ya fedha katika mradi huo hairidhishi, huku akibainisha kuwa kupitia vyanzo vya ndani watatenga shilingi milioni 172 kwa ajili ya kukamilisha machinjio hiyo.
Machinjio hiyo ilianza kujengwa mwaka 2018 na ilitazamiwa kukamilika mwaka2019 na kuanza kutoa huduma lakini maendeleo yake yamekuwa yakisuasua na kusababisha baadhi ya viongozi kuilalamikia.