Na Anitha Jonas - COSOTA,Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa awatoa hofu Wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha kwa kuelezea kuwa Serikali imeandaa mifumo ya kidijitali ambayo itarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo na kuongeza gawio.
 
Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 08, 2021 katika kikao chake na  Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Muziki na Filamu nchini kilicholenga kuzungumzia Kanuni ya 26 ya BASATA inayohusu uhakiki wa kazi za Muziki na Filamu  kabla ya kuingia sokoni au kusambazwa.
 
"COSOTA imekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mirabaha kutokana na uhaba wa watumishi hivyo kwa kupitia mfumo mpya wa kidijitali utakao anzishwa hivi karibuni utarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo, Serikali inataka kutoa gawio la pesa nyingi kwa wasanii na siyo fedha kidogo hivyo tunawaomba mvumilie kidogo kuanzia mwaka mpya wa fedha mambo yatakuwa mazuri,"Mhe.Bashungwa.
 
Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho Waziri huyo alitoa maelezo mahususi kwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) akiwataka kusitisha utekelezaji wa Kanuni ya 26 inayotaka kazi zote za Muziki kukaguliwa nao kabla ya kusambazwa.
 
Aidha, Mhe.Bashungwa alisisitiza kuwa maelekezo hayo ya kusikitishwa kwa matumizi ya Kanuni hiyo ni kwa upande wa Muziki pekee ila kwa upande wa Filamu itaendelea kutumika kama kawaida.
 
Pamoja na hayo Mhe.Bashungwa aliendelea kutoa maelekezo ya haraka kwa BASATA kwa kuwataka kuanzisha mchakato wa kurekebisha Kanuni hiyo kwa kuwashirikisha wadau  hao wa vyama na mashirikisho ili kuweza kupata Kanuni mpya isiyodumaza tasnia ya Muziki lakini izingatie maadili ya taifa.
 
Halikadhalika Waziri huyo ameelekeza BASATA kwa kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo utakao kuwa kukitoa dira njema ya uendeshaji na ukuzaji wa tasnia ya Muziki.
   
Naye mmoja wa wasanii hao Soggy Doggy alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maamuzi  aliyoyafanya na kumpongeza na kuahidi kuendelea kushirikiana na wasanii wa Muziki katika  kukuza na kuiendeleza tasnia ya Muziki nchini.
*****MWISHO*****