Watumishi Sekta Ya Uvuvi Watakiwa Kubuni Teknolojia Za Kuwasaidia Wadau Wa Uvuvi
Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amewataka watumishi wa wizara hiyo Sekta ya Uvuvi kubuni teknolojia za kisasa zitakazoleta tija kwa wadau wa uvuvi na taifa kwa ujumla.
Akizungumza jana (10.05.2021) wakati akifunga mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Uvuvi uliofanyika jijini Dodoma, Mhe. Ulega amesema ni wakati sasa kwa watumishi wa sekta hiyo kuwa wabunifu zaidi ili wavuvi wa Tanzania Bara na Visiwani waweze kufanya shughuli zao kwa njia za kisasa zaidi.
“Nataka muwe wabunifu na myafanyie kazi kwa haraka zaidi nina imani mtakuwa mnakimbizana ili kuwasaidia wavuvi wa taifa hili bara na visiwani kwa kutumia teknolojia ili nchi ione kweli sasa hawa watu wameamua kwa dhati kabisa kuja na mambo mapya.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha, amesema mkutano huo una lengo la kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inapata manufaa zaidi na kuhakikisha wadau wananufaika na matarajio yake ni kwamba wajumbe wa mkutano huo watakuwa wamejadili kwa kina mambo ya msingi ambayo yatakuwa na manufaa.
“Siyo matarajio yetu muache mkutano wa namna hii kuzungumza mambo kwa uwazi badala yake kutumia mikutano isiyo rasmi kwa kuwa tu labda haupati nafasi ya kusema.” Amefafanua Mhe. Ulega
Pia, ametoa rai kwa menejimenti ya Sekta ya Uvuvi kwamba yale yote yaliyojadiliwa kwenye mkutano wa Baraza la wafanyakazi Sekta ya Uvuvi yaratibiwe vizuri ili kila mtumishi ambaye hakupata nafasi ya kushiriki aweze kupata mrejesho na makubaliano au maazimio ya mkutano huo pamoja na kutaka mkutano ujao uwe na taarifa ya utekelezaji wake.
Naibu waziri Ulega amewakumbusha pia watumishi wa wizara hiyo Sekta ya Uvuvi kufanya kazi kwa ueledi mkubwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa vinakandamiza utoaji wa haki.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Uvuvi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema mkutano huo umekuwa na mada mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha zinaboresha utendaji kazi wa watumishi na namna bora ya kuwahudumiwa wadau wa sekta hiyo.
Amebainisha kuwa lengo la baraza hilo ni kuhakikisha linakuwa na mikutano ya mara kwa mara kutokana na takwa la kisheria ili iweze kutatua changamoto mbalimbali zikiwa katika hatua za awali.
Nao baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Uvuvi wakizungumza katika mkutano huo wameonesha kuridhishwa kwa uwepo wa baraza hilo ambalo limefanya mkutano wake wa kwanza tangu liundwe, wakidai kuwa kupitia baraza wataweza kufikisha maswali na maoni mbalimbali yanayohusu watumishi na wadau wa Sekta ya Uvuvi.
Wameuomba uongozi wa wizara kuhakikisha unaendelea kulinda maslahi ya wafanyakazi pamoja na kuwahakikishia usalama wao wanapokuwa maeneo mbalimbali ya kazi ambayo yanahitaji uangalizi maalum.