Zaidi ya watu 150 wamejeruhiwa usiku wa kuamkia leo wakati wa makabiliano baina ya waumini wa Kipalestina na maafisa polisi wa Israel katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem . 

Takribani Wapalestina 163 wamejeruhiwa na maafisa 6 wa polisi wa Israel nao wameripotiwa kujeruhiwa katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa na kwingineko Mashariki mwa Jerusalem. 

Polisi wa Israel walitumia risasi za mipira kukabiliana na waumini wa Kipalestina waliokuwa wakirusha mawe, chupa na fataki.Polisi pia walilifunga lango la kuelekea msikiti wa Al-Aqsa ndani ya mji wa zamani huko Jerusalem.