Abiria 87  wakiwepo wafanyakazi 25 wa meli ya MV Mbeya II wamenusurika kifo baada ya meli hiyo kupigwa na mawimbi ikiwa safarini katika Ziwa Nyasa na kukwama kwenye mchanga karibu na Bandari ya Matema.
 

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta, amesema kuwa tukio hilo limetokea jana Jumatatu Aprili 3, 2021 majira ya saa 12 jioni.

Kitta amesema kuwa baada ya kupata taarifa waliongozana na kamati ya ulinzi na usalama na kukuta meli hiyo ikiwa imetitia katika Bandari ya Matema na kwamba hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza.

Amesema kwa sasa huduma za usafiri za meli hiyo zimesitishwa, ili wataalam waweze kuifanyia uchunguzi.

Mbali na kubeba abiria, meli hiyo pia ilikuwa imebeba tani 12 za mizigo.