Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Charles Msonde, amesema kuwa mitihani ya kidato cha sita Tanzania Bara na Visiwani itaanza kesho Mei 3 hadi Mei 25, 2021.

Taarifa hiyo ameitoa hii leo Mei 2, 2021, jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa licha ya mitihani hiyo pia itafanyika mitihani ya ualimu, ambapo vituo katika shule za sekondari ni 804, vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 248 na kwa upande wa vyuo vya ualimu viko 75 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

"Jumla ya watahiniwa 90, 025 ndiyo waliosajiliwa kufanya mtihani huo wa kidato cha sita na kati yao watahiniwa wa shule wako 81,343 na wakujitegemea wako 8,682, na kati ya watahiniwa hao wa shule wanaume ni 46,233 na wanawake 35,110", ameeleza Dkt. Msonde