Baadhi ya raia walioyatoroka makaazi yao baada ya mlipuko wa volkano uliotokea usiku wa kuamkia jana huko mjini Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wameanza kurejea katika majumba yao kutokana na hali ya ukosefu wa chakula katika maeneo waliyokimbilia. 

Kwa sasa mitetemeko midogo ya ardhi na ongezeko la joto ndiyo mambo yanayoendelea kushuhudiwa licha ya moto uliotokana na volkano kuonekana kuanza kupungua. Maelfu ya watu wameyakimbia makaazi yao baada ya mlima Nyiragongo kulipuka usiku wa kuamkia jumapili. 

Mara ya mwisho mlima huo kulipuka ilikuwa Januari 17 mwaka 2002 ambapo zaidi ya watu mia moja walipoteza maisha na tope la Volcano lilienea karibu Goma mashariki yote ikiwemo nusu ya eneo la kutua ndege katika uwanja wa ndege wa mji huo.