Mfuko wa Taifa la Bima ya Afya (NHIF) umetangaza kuongeza kundi la wategemezi katika huduma zake kutoka umri wa miaka 18 hadi miaka 21.

Katika taarifa ya mfuko huo iliyotolewa leo Jumatano Mei 5, 2021 na meneja uhusiano, Anjela Mziray inaeleza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa katika sherehe za Mei Mosi, 2021 zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ameainisha kuwa Rais Samia alieleza kuwa kusudio la Serikali ni kuyajumuisha mabadiliko hayo kwenye mabadiliko ya sheria ya mfuko wa Bima ya Afya yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

"Kutokana na maelekezo hayo, mfuko unapenda kuwataarifu umma na wanachama wake kwamba umepokea maelekezo hayo kama yalivyotolewa na umeanza kukamilisha taratibu za ndani ikiwa ni pamoja na marekebisho ya mifumo wakati mchakato wa marekebisho ya sheria ukiendelea.”

"Pia mfuko utatoa taarifa rasmi kwa umma na wanachama wakati mchakato huo ukiendelea," anaeleza taarifa hiyo.