Na Beatrice Sanga, MAELEZO.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC kimeanza kufanya maboresho ya huduma za uwekezaji  kwa kuunganisha mifumo ya kielektroniki kwa taasisi na idara 11 za Serikali zinazotoa huduma za mfumo wa mahala pamoja lengo likiwa ni kurahisisha utoaji wa vibali na leseni za uwekezaji kwa kuunganisha mifumo hiyo ili kuwa na dirisha moja la uwekezaji nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Maduhu Kazi amesema maboresho hayo yatasaidia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma za wawekezaji na kuimarisha utendaji kazi wa kituo hicho ikiwa ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alilolitoa Aprili, 2021 wakati akiwaapisha makatibu wakuu wa Wizara.

Dkt Maduhu amefanya kikao cha pamoja na  wakuu wa Taasisi na Idara za Serikali 11 zinazotoa huduma kwenye Kituo cha huduma kwa wawekezaji cha mahali pamoja (One Stop Facilitaion Centre) na kubainisha kuwa mchakato wa maboresho hayo unaendelea kufanyiwa kazi.

“Kama mnavyofahamu, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ya namna ya kuboresha huduma za uwekezaji, kikao hiki ni muendelezo wa utekelezaji wa majukumu hayo, tulishaanza kuyafanyia kazi, na sasa tunaendelea, lengo ni kutoa huduma bora zaidi za uwekezaji” amesema Dkt. Maduhu.

Katika kikao hicho, Dkt. Maduhu amepokea taarifa ya hatua ambazo zimechukuliwa kwa kila Taasisi na Idara husika zikiwepo kila taasisi kufungua mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya utoaji vibali na leseni mbalimbali, kuunganisha mifumo hiyo ili kuwa na dirisha moja la huduma kwa wawekezaji nchini na taasisi husika kukamilisha hatua zote ikiwepo kuchambua na kutoa maamuzi kwa maombi husika ya wawekezaji.

Maboresho haya yanaelezwa kuwa yatawawezesha wawekezaji wanaowekeza nchini kupata huduma kwa muda mfupi na kwa kutumia gharama ndogo.

Baadhi ya Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Uhamiaji, Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), Mamlaka ya Mapato Tanzani (TRA), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira  (NEMC), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) naOfisi ya Waziri Mkuu (Kazi).