Wahudumu wa afya wapatao 115,000 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona.
Takwimu hizo zimetolewa na mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliyesifu ari ya kujitolea ya wahudumu wa afya kote ulimwenguni katika kukabiliana na janga la Covid-19.
Tedros ameongeza kuwa wafanyakazi wengi wa afya tangu kuanza kwa janga hili wamehisi kuchanganyikiwa, kuwa wanyonge na wasio na kinga, ukosefu wa upatikanaji wa vifaa vya kinga binafsi na chanjo.
Aidha mkurugenzi huyo ameelezea ukosefu wa chanjo kama kashfa akionya kuwa ni kuendeleza janga hilo. Zaidi ya asilimia 70 ya chanjo zote za Covid-19 zimekwenda kwenye nchi 10.
Amehimiza nchi zenye shehena kubwa ya chanjo kuzigawa na kuonyesha ushirikiano mkubwa utakaoongeza uzalishaji na usambazaji wa chanjo.