Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limezitaka nchi tajiri kuacha kuwapa watoto chanjo ya Covid-19, na badala yake kuzipeleka dozi hizo katika nchi masikini, likionya kuwa yaelekea mwaka wa pili wa janga la virusi vya corona utakuwa na vifo vingi zaidi ya mwaka wa kwanza. 

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema inakatisha tamaa kuona mataifa tajiri yakiwachanja vijana na watoto wadogo, wakati nchi zinazoendelea bado hazijaanza kutoa huduma hiyo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya. 

Tedros amesema nchi zilizoendelea zinapaswa kuchangia dozi za chanjo kupitia mpango wa kimataifa wa chanjo kwa wote wa Covax, kuhakikisha kuwa zinawafikia wanaozihitaji kwa hali ya dharura. 

Kulingana na takwimu za shirika la habari la AFP, kati ya dozi bilioni 1.4 za chanjo ya Covid-19 zilizokwishatolewa kote duniani, asilimia 44 imekwenda katika nchi tajiri ambazo wakaazi wake ni asilimia 16 ya watu wote ulimwenguni.