Na Mathew Kwembe, Dodoma
Serikali imetenga shilingi milioni 61 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita moja pamoja na ujenzi wa makalvati 14 katika mwaka wa fedha 2021/22.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe Zuena Athumani Bushiri, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.David Silinde amesema serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika bajeti zijazo ili kuiboresha na kurahisisha usafirishaji wa Jasi.

Amesema kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha barabara hii inapitika muda wote na ndio maana imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara.

Naibu Waziri amesema katika mwaka wa fedha 2019/20 Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Same umefanya matengenezo ya barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi maeneo korofi yenye urefu wa kilomita 3.5 kwa gharama ya Shilingi milioni 77.3.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/21 TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Same   imefanya matengenezo ya barabara hiyo kipande chenye urefu wa kilomita mbili kwa kiwango cha Changarawe kwa gharama ya Shilingi milioni 49.4.

Barabara ya Makanya hadi kwenye machimbo ya Jasi Wilayani same ina urefu wa kilomita 40.9. Kipande cha kilomita 4.5 cha barabara hii kimeinuliwa kwa kujengwa tuta kati ya kilomita 14.5 zinazotakiwa kujengwewa tuta kwa kiwango cha changarawe.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mhe.Silinde amesema katika mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2020/21 barabara za kutoka Rubanga, Isurwa, Butundwe, Mkoba, Kukuruma, Kamhanga, Kishinda na Mkorani zimetengewa Shilingi milioni 318.8 kwa ajili ya matengenezo ya kilometa 33 na wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa kazi.

Amesema matengenezo ya barabara hii yanatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2021 na kuwa vijiji vilivyotajwa vinaunganishwa na barabara za Mkoba bridge – Isulwabutundwe – Lubanga yenye urefu kilomita 15  na Geita – Isamilo – Mkolani (Busekeseke) yenye urefu wa kilomita 18 ni barabara muhimu sana wananchi.