Mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu,  Gerson Msigwa amewataka Watanzania kupuuza taarifa zilizorushwa na televisheni moja ya nchini Kenya kwamba Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu ameagiza wafungwa kwa kisiasa nchini kuachiwa huru.

Msigwa ametoa ufafanuzi huo leo Ijumaa Mei 7,2021 muda kabla ya kuanza kwa mkutano wa Rais Samia na wazee wa Dar es Salaam unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.

"Nchi yetu itambulike haina wafungwa wa kisiasa lakini pia video ile inaeleza rais amemuagiza mwanasheria mkuu wa Serikali awaachie wafungwa 23 ambao hawapo, Rais haingilii uhuru wa mahakama na hizi ni shughuli za kimahakama zinafanywa na mahakama, na la tatu mwanasheria mkuu wa Serikali haendeshi shughuli kama hizo mahakamani.”

"Kupitia nyie waandishi wa habari ningependa Watanzania wapuuze habari hizo hazina ukweli wowote, chombo cha habari cha nchi jirani nisingependa kukitaja naamini kwamba watazingatia weledi wao na kuomba radhi na kufuta hiyo taarifa yao ambayo wameieneza kwenye chombo chao cha habari," amesema Msigwa. 

Amesema kuwa hatua mbalimbali za kisheria zinafuatwa, kufuatia usambazwaji wa taarifa hizo za uongo.