Rais wa Jamuhuri ya Kidemkrasia Congo Felix Tshisekedi amesema hali nchini humo ni shwari baada ya serikali kutangaza kimakosa mlipuko mwengine wa Volkeno. 

Kauli ya Tshisekedi inakuja baada ya wakimbizi zaidi ya 1000 kuondoka katika kambi nchini Rwanda na kurejea nchini Congo.Mapema hapo jana serikali ilitangaza kuripuka kwa Volkeno nyengine lakini baadaye ilikiri kuwa tangazo hilo halikua sahihi. 

Wiki moja baada ya Mlima Nyiragongo kuripuka tena, na kusababisha uharibifu na uhamisho mkubwa, rais Tshisekedi amesema hali ni mbaya lakini imedhibitiwa. 

Haya yanajiri wakati ambapo serikali ya Congo inazidi kukosolewa juu ya mzozo mkubwa wa kibinaadamu unaoweza kutokea kutokana na mripuko wa Volkeno.

Shirika linalofuatilia mienendo ya milima ya Volkeno katika mji wa Goma limethibitisha kuwa kuna matukio makubwa yanayoendelea katika mlima Nyamuragira lakini mpaka sasa hakujatokea mlipuko.