RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza haja kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar kushirikiana vyema na Chama cha SKAUTI Tanzania ili kuwajengea vijana uwezo mzuri wa stadi za maisha pamoja na uzalendo.


Rais  Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Uongozi wa Chama cha SKAUTI Tanzania ukiongozwa na kiongozi wake Mkuu Hajjat Mwantumu Bakari Mahiza akiwa amefuatana na viongozi kutoka Zanzibar.


Alisema kuwa kuna vijana wengi wa SKAUTI waliohamasika katika chama hicho hapa Zanzibar hivyo, ni vyema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ikashirikiana  na chama hicho katika kuhakikisha vijana hao wanatekelezewa mahitaji yao kutokana na shughuli wanazozifanya.


Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa programu za vijana ambazo tayari zimeshafanyika kwa upande wa Tanzania Bara ni nzuri na zinahitajika hasa kwa vijana na kueleza kwamba kuna vijana wengi wamehamasika kujiunga na chama hicho hivyo, ni vyema wakatumiwa vizuri ili lisijekuwa jeshi la kufanya mambo mabaya hapo baadae.


Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba programu hizo zifanywe japo kwa awamu kutokana na uwezo uliopo wa kifedha kwa Wizara ya Elimu ili vijana waweze kupata mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika stadi zao wa maisha.


Rais Dk. Mwinyi pia, alitoa maelekezo ya kurejeshewa kwa ofisi zake zilizokuwa zikitumiwa na chama hicho hapa Zanzibar ili chama hicho kiweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.


Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema kwa Wizara ya Elimu kutafuta njia ya kukutana na vijana hao wa SKAUTI huku akieleza haja ya Wizara hiyo kuwawezesha vijana wa SKAUTI kufanya programu hizo.


Rais Dk. Mwinyi pia, alipokea pongezi za ushindi wake uliomuwezesha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutoka kwa uongozi huo wa SKAUTI.