Rais wa Mali Bah Ndaw na waziri mkuu Moctar Ouane wanaendelea kushikiliwa kizuizi katika kambi ya jeshi, walikopelekwa jana baada ya kutangaza mabadiliko katika baraza la mawaziri yaliyowakasirisha wanajeshi.
Katika mabadiliko hayo, maafisa wawili wa jeshi waliohusika katika mapinduzi yaliyoiangusha serikali ya kiraia miezi tisa iliyopita waliondolewa katika nyadhifa zao.
Umoja wa Afrika, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS wametaka viongozi hao waachiwe huru bila masharti yoyote.
Katika tangazo la pamoja lenye maneno makali, jumuiya hizo zimetoa onyo, zikisema mwanajeshi yeyote aliyechangia katika tukio hilo lililotajwa kuwa jaribio la mapinduzi, atawajibishwa binafsi kuhusiana na usalama wa viongozi hao waliokamatwa.
Aidha, tangazo hilo limesema ujumbe wa Jumuiya ya Ecowas utawasili nchini Mali Jumanne. Hadi sasa jeshi la Mali halijatoa tamko lolote kuhusiana na hatua yake hiyo.