Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo  amemkabidhi nyumba ya kuishi Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete iliyojengwa katika Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam.

Nyumba hiyo imejengwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba 12 cha Sheria ya mafao ya hitimisho la kazi kwa viongozi wa siasa, sura ya 225 na marejeo ya mwaka 2020 ambayo pamoja na stahili zingine za matunzo ya viongozi wakuu wastaafu inaelekeza kuwa Rais anayestaafu anastahili kujengewa nyumba ya kuishi yenye hadhi ya Rais.

Akizungumza baada ya kukabidhi nyumba hiyo, Rais Samia amempongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa kupata makazi hayo na amemhakikishia kuwa Serikali itaendelea kumtunza yeye na viongozi wengine wastaafu kama inavyoelekezwa katika sheria.

Amebainisha kuwa Serikali itafanyia kazi uboreshaji wa sheria hiyo pamoja na kuhakikisha wajane/wagane wa viongozi wanatunzwa.

Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa kuanza maandalizi ya kutimiza haki zote anazostahili aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri Mchengerwa amesema nyumba hiyo ni ya 3 kukabidhiwa ikitanguliwa na nyumba ya Rais Mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa na Rais Mstaafu Dkt. Ali Hassan Mwinyi na kwamba nyumba ya Baba wa Taifa Hayati Mw. Julius Kambarage Nyerere ilijengwa na kukabidhiwa kwake na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika shukrani zake, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Salma Kikwete ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutekeleza takwa hilo la kisheria, ameishukuru TBA kwa kukamilisha ujenzi tangu ulipoanza mwaka 2018 na amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kumkabidhi nyumba hiyo.

Rais Mstaafu Kikwete amempongeza Mhe. Rais Samia kwa uongozi wake tangu alipopokea kijiti kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwani nchi imetulia, mambo yanakwenda na watu wana matumaini makubwa nae.