Rais Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Balozi Xia Huang jijini Nairobi, Kenya.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Huang amewasilisha salamu za pole za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwa Rais Samia kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli na kumpongeza kwa kupokea kijiti cha urais, akiwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Tanzania.

Pia, Balozi Huang ameipongeza Tanzania kwa mchango na ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa umoja wamataifa katika juhudi za kulinda amani na kuimarisha usalama katika maeneo yote yenye mapigano na makundi yanayohasimiana na ameahidi kuwa umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania kulinda amani ili maendeleo ya jamii na ustawi yastawi.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema hali ya ulinzi na usalama na demokrasia nchini Tanzania ni nzuri na ameomba umoja wa mataifa kuendeleza jitihada za kulinda amani na usalama katika maeneo yote yenye matatizo na kuushawishi Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa Burundi.