Na.WAMJW-Dsm
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi amewataka maafisa Afya katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na makampuni ya kifedha yanayotoa huduma za kupokea malipo kwa Abiria wanaowasili nchini na kufanyiwa vipimo vya Covid 19, kufanya kazi kwa ushirikiano na ufanisi, ili kuweza kutoa huduma yenye ubora na kutowachelewesha Abiria wanaopatiwa huduma katika Uwanja huo.

Prof Makubi amesema hayo katika ziara yake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,yenye lengo la kukagua huduma za upimaji wa Covid 19 kwa abiria wa wanaowasili nchini zinazotolewa na maafisa Afya wa uwanja huo na kuangalia changamoto zinazopelekea kuwepo kwa ucheleweshaji wa huduma kwa abiria hao kama zimefanyiwa kazi.

Katibu Mkuu amesema kitendo cha kuchelewesha kutoa baadhi ya huduma kwa baadhi ya abiria wanaowasili nchini kamwe hakivumiliki, hivyo watendaji wanaohusika wajaribu kuondoa vikwazo vinasababisha kuchelewesha huduma hizo, ambazo zimekuwa kero kwa baadhi ya abiria wanaowasili nchini na kutakiwa kufanyiwa vipimo vya Covid 19 uwanjani hapo.

“Kweli kuna ucheleweshaji unaoweza kufanyika na mtu akakuvumilia wala asikereke lakini ikishafika masaa mawili hiyo haikubaliki, hebu tuondoe hivi vikwazo vinavyosababisha huduma kuchelewa ili wananchi waweze kupata huduma na tusionekane kero kwao” Alisema Prof Makubi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale amemuondoa hofu katibu Mkuu katika kusimamia huduma zinazotolewa katika Uwanja huo, ambapo amesema atahakikisha anasimamia maafisa Afya uwanjani hapo na kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na watashirikiana na wadau wengi katika kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanapata huduma zenye kiwango cha ubora wa juu.