Na Eliud Rwechungura
Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amewahakikishia Wafanyabiashara kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ili kuhakikisha wanafanikiwa huku akiwahasa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kuzingazia Sheria na taratibu zilizowekwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuondokana na vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwekwa  kutoka na kutozingatia Sheria na taratibu za kufanya biashara mipakani.

Prof. Mkumbo ameyasema hayo 30 Mei 2021 alipoambatana na Mawaziri wa Kenya na Tanzania kutembelea Mpaka wa Namanga kujionea jinsi biashara na shughuli za upitishaji wa bidhaa na huduma zinafavyofanyika katika Mpaka huo baada ya nchi hizo kukubalina kuondoa vikwazo 30 vya biashara visivyokuwa vya kiushuru.

“Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anataka kuona Maisha ya Watanzania yanaboreka na biashara zinafanyika vizuri, niwahakikishie wafanyabiashara wa Watanzania, Serikali yenu ipo na nyie na itaendelea kuwaunga mkono na kuwapa msaada ili kuona mnafanikiwa lakini kwa upande wenu tunaomba katika kufanya kwenu biashara mzingatie sheria na taratibu zilizopo kwasababu nchi zetu zinaongozwa na utawala wa sheria” ameeleza Prof. Mkumbo

Ameongeza kuwa, lengo la ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Waheshimiwa Marais wa Tanzania na Kenya ya kuhakikisha mahusiano ya wananchi wa nchi mbili yanaboreka lakini muhimu Zaidi biashara hazikwami ndo maana wamekutana Mawaziri kutatua mambo mengi yaliyokuwa yanakwamisha biashara ikiwemo changamoto ya mahindi hapa mpakani wameweza kuizungumzia  na anashukuru imetatuliwa na mambo mengine mengi yalikuwepo pande zote mbili za Tanzania na Kenya.

Aidha, Prof. Mkumbo amewapongeza wataalam wa pande zote mbili za Tanzania na Kenya kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya huku akiwahasa kuendelea kuimalisha mahusiano mazuri kwa kukaa Pamoja na kujadiliana kwa kuzitatua changamoto kwasababu ni jambo kubwa na la muhimu viongozi wetu wanalotaka kuliona

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiliamali nchini Kenya Mhe. Betty Maina amefurahishwa na kuona changamoto 30 kati ya 64 zimetatuliwa na hizo nyingine zilizobaki wamejiwekea muda wa miezi mitatu kuzifanyia kazi huku akiwataka wafanyabiashara wa pande mbili kuendelea kuzingatia sheria ambazo zimewekwa kwa pande zote mbili za Kenya Tanzania wakati wa ufanyaji biashara.