Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), inaandaa Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yatakayofanyika tarehe 28 Juni, hadi 13 Julai, 2021 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Lengo la Maonesho haya ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi pamoja na taasisi mbalimbali kutangaza biashara ya bidhaa na huduma, kujifunza uzalishaji bora wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa na kutengeneza mitandao ya mawasiliano baina yao itakayowasaidia kukuza biashara na kupata wabia kwenye biashara zao, ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu”. Kauli mbiu hii inalenga kutambua mchango wa Sekta ya Viwanda katika kuchochea uzalishaji kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi ili kukuza biashara ya ndani na nje, kuongeza ajira na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa

Sambamba na Maonesho haya, Mikutano ya Kibiashara (B2B) itafanyika kwa njia ya mtandao (Zoom Meetings ) ili kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini yakiwemo mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini.

Aidha kutakuwa na huduma ya Kliniki ya Biashara, kwa wafanyabiashara ili kuboresha na kuimarisha mazingira wezeshi ya ukuaji endelevu wa biashara nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa teknolojia rahisi na za kisasa

Pamoja na maonesho ya jumla ya bidhaa mbalimbali maonesho ya mwaka huu yatakuwa na maeneo matatu ya upekee kama ifuatavyo:-

Eneo maalum litakalojulikana kama Kilimo Zone. Eneo hili litatumiwa na Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo kama vile bodi za mazao, wazalishaji wa pembejeo na teknolojia za kilimo pamoja na wadau wengine wa kilimo walioko ndani ya nchi ili kurahisisha upatikanaji wao katika eneo moja na kuwaunganisha wazalishaji wa bidhaa hizo na masoko endelevu. Aidha, washiriki katika banda hili watapata fursa ya kushiriki Mikutano ya Kibiashara kwa njia ya mtandao (Zoom Meetings) ili kuunganishwa na wadau wa biashara ya mazao ndani na nje ya Nchi kwa lengo la kuunganishwa na masoko pamoja na Teknolojia mbalimbali.

Pia kutakuwa na mtaa wa madini utakaowashirikisha Wadau wote wa Sekta ya Madini ambao ni pamoja na Wachimbaji Wadogo na Wakubwa, Watafiti na Masonara ili kupanua fursa za masoko katika Sekta hii muhimu katika uchumi; na kutoa taarifa mbalimbali kuhusu rasilimali hiyo kwa watembeleaji wa Maonesho. Pamoja na

Pamoja na mtaa wa viwanda vidogo vidogo na wajasiriamali kwa ajili ya kutoa fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi

Pamoja uwepo wa changamoto ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid -19) unaoikabili dunia, hadi sasa nchi zipatazo saba (7) zimethibitisha kushiriki. Nchi hizo ni pamoja na China, Ghana, Kenya, Pakistan, Syria, India na Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu (UAE). Makampuni yapatayo 54 kutoka nje ya nchi na 2,803 ya ndani ya nchi yamethibitisha kushiriki.

Hivyo, naendelea kuwahamasisha Jumuiya ya Wafanyabiashara, Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na watoa huduma mbalimbali kutoka ndani na nje ya Nchi kujiandikisha kushiriki Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, ili kutumia jukwaa hili. Serikali imeandaa mazingira yatakayomwezesha mfanyabiashara kujenga mtandao mpana wa biashara.

Usajili unafanyika kupitia tovuti ya TanTrade ambayo ni https://bit.ly/3heHRxP au unaweza kutembelea Ofisi za TanTrade zilizopo katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl J.K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.