Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelaani ongezeko la vurugu kati ya Israel na Waplestina akisema ni jambo lisilokubalika, huku akitaja vifo vya watoto kuwa ni ishara ya kuharibu mustakabali wao wa baadae. 

Papa Francis ameyasema hayo wakati wa ibada ya Jumapili na kuombea amani, utulivu na msaada wa jumuiya ya kimataifa katika kufungua njia ya majadiliano. Kiongozi huyo amesema hakuna amani inayopatikana kwa kuwaua binadamu wengine. 

Wito huo unakuja wakati mashambulizi ya Israel yakiwaua Wapalestina 40 katika ukanda wa Gaza. Israel imesema wimbi la mashambulizi yake ndani ya saa 24 zilizopita umeyapiga maeneo 90 ya Gaza. 

Jeshi la Israel limedai kwamba karibu maroketi 3,000 yamerushwa kutokea ukanda wa Gaza kuelekea Israel, idadi ambayo ni kubwa kuripotiwa na kati yake 450 yalianguka ndani ya mipaka ya Gaza.