Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, vina wajibu wa kuweka mawakala kwenye vituo vya kupigia na kujumlisha kura lakini mawakala hao na wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia Sheria za Uchaguzi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2021 na kushirikisha kata za Buziku (Halmashauri ya Wilaya ya Chato), Bugarama (Halmashauri ya Wilaya ya Geita), Igunga (Halmashauri ya Wilaya ya Igunga), Ligoma (Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru) na Kata ya Miuta iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

Amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye majimbo na kata zinazofanya uchaguzi huo.

Jaji Mst. Kaijage amesema Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.

Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na kata tano za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua wabunge na madiwani wanaowataka.

Amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zinakamilika leo jioni saa 12:00 hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.

“Pili upigaji kura utafanyika katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni”alisema Jaji Mst. Kaijage na kuongeza:

“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye majimbo na kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Kifungu cha 62 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.”

“Mojawapo ya vitambulisho mbadala ambavyo mpiga kura anaweza kutumia ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika  ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura anapokwenda kupga kura. Aidha majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala”

Jaji Mst. Kaijage amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nuktanundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze kupiga kura wenyewe.

Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.

Amewakumbusha wapiga kura kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka jana yaliyokubaliwa na wahusika wote vikiwemo vyama vya siasa, kuwa wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura, hivyo Tume imewashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, itahusisha idadi ya wapiga kura watakaopiga kura 303,965  walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kupigia kura ni vituo 793.