Israel inakabiliwa na mgogoro unaoendelea kufukuta kutoka pande mbili, ikipambana kutuliza vurugu kati ya Waarabu na Wayahudi kwenye mitaa yake baada ya siku kadhaa za makabiliano makali na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. 

Licha ya juhudi za kidiplomasia za kusitisha machafuko, ambayo Rais wa Marekani Joe Biden amesema anatumai yatasitishwa bila kuchelewa, mamia ya maroketi yamevurumishwa katika anga za Gaza usiku kucha. 

Watu 83 wameuawa mpaka sasa katika Ukanda wa Gaza, wakiwemo watoto 17. 

Kundi la Hamas linaloutawala ukanda wa Gaza limetangaza kifo cha mkuu wa majeshi katika mji wa Gaza, Bassem Issa, huku jeshi la Israel likisema limewauwa maafisa wengine watatu waandamizi. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tayari limefanya vikao viwili vya faragha kwa njia ya video, huku Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel, ikipinga kutolewa tamko la pamoja ambalo ilisema halitaweza kutuliza hali.

-DW