Vijana nchini wameshauriwa kujikita kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa njia ya kilimo hai kwa kutotumia kemikali hali inayowapatia uhakika wa masoko kutokana na ubora wa mazao hayo kiafya.


Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa kikundi cha vijana Tugende na Twiyunde vya  Kata ya Msufini wilaya ya Morogoro wanaolima mazao ya viungo kwa kutumia kilimo hai Mkurugenzi wa shirika la Kilimo Endelevu Janet Maro aliwahakikishia soko vijana hao.


“Bidhaa za kilimo hai zina uhakika wa soko kutokana na faida zake kiafya na pia kuwa na mwonjo mzuri unaovutia walaji  kutokana kuzalishwa bila kutumia kemikali za viwandani .SAT tutanunua mazao yenu kwa ajili ya kuongeza thamani na kuyafikisha kwa walaji ndani na nje ya nchi“ alisema Janet.


Taarifa ya vikundi hivyo iliyotolewa na Meneja miradi wa SAT Morogoro Vijijini Joel Paul ilisema tayari katika mwaka huu 2021 jumla ya tani 146 za tangawizi iliyozalishwa na vikundi kwa njia ya Kilimo hai inatarajiwa kuvunwa na kunuliwa na shirika hilo tofauti na tani 28 zilizozalishwa mwaka 2018 wakati mradi wa Kilimo cha viuongo ulipoanza.


Joel alisema vijana hao wapatao 368 katika kata ya Mkuyuni wanazalisha mazao ya viungo ikiwemo karafuu kwenye safu za milima ya Urugulu, tangawizi, mdarasini, pilipili, pilipili manga, hoho,binzari ambapo uzalishaji umeongezeka kufuatia elimu ya kilimo hai waliyopatiwa na watalaam wa shirika la SAT.


Kuhusu vikundi vingi kuwa na wasichana kuliko vijana wa kiume , Mkurugenzi huyo alisema shirika la SAT limechagua kusaidia vijana hususan wasichana wakina mama wadogo kuwafundisha kilimo hai na ujasiliamali ili wajiajili na kutunza familia zao.


Janet alisema kwa mujibu wa utafiti waliofanya ulionyesha mkoa wa Morogoro na Dodoma zina wasichana wengi waliozaa mapema na kukosa uhakika wa matunzo kwa watoto wao hivyo kupitia mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) unatoa fursa ya ujasiliamali, kilimo hai hususan mazao ya bustani ,mpunga na viungo.


Kwa upande wake Mratibu wa Mkakati wa Vijana Kushiriki kwenye Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Revelian Ngaiza aliwapongeza vijana kwa kujiunga kwenye vikundi kwa ajili ya kazi za kilimo zenye uhahika wa ajira kutokana na uhitaji wa mazao ya chakula na biashara.


Ngaiza alisema vijana ndio nguvu kazi hivyo wakitumia fursa ya uwepo wa ardhi na teknolojia rahisi ya Kilimo hai watazalisha kwa tija na kuwa na uhakika wa kipato hivyo kuzalisha ajira mbapo ndio lengo la mkakati huo.


“Serikali inapenda kuona vijana wakijiunga pamoja kwenye vikundi ili kutumia fursa ya nguvu walizonazo kuzalisha mazao ya kilimo kwa lengo la kujiajili, ndio maana kupitia halmashauri vikundi vya vijana na akina mama vinapatiwa mikopo kwa ajili ya ujasiliamali ikiwemo kazi za kilimo” alisema Ngaiza.


Shirika la SAT la Morogoro linafanya kazi ya kutekeleza mkakati wa Taifa wa Vijana kushiriki kwenye sekta ya kilimo unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo ambapo lengo ni kuwafundisha kufanya kilimo kinachozingatia afya ya mimea, wanyama, mazingira na baionowai (Kilimo hai) na matumizi ya mbegu bora zenye kuwahakikishia mazao mengi na bora.


Mwisho
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo