Kamati ya kitaalamu iliyoundwa kufanya tathmini ya hali ya ugonjwa wa corona nchini, imetoa mapendekezo 19 ikiwamo matumizi huru ya chanjo ya ugonjwa huo, ili kutoa fursa ya kinga kwa makundi maalumu kama wazee, wenye magonjwa sugu na wahudumu wa afya.


Kamati hiyo pia imebaini kuwa chanjo hizo zina ufanisi na usalama unaokubalika kisayansi na kwamba kabla ya kutolewa kwa makundi hayo kwanza zifanyiwe uchunguzi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Said Aboud, akikabidhi ripoti ya kamati hiyo jana kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu, jijini Dar es Salaam, alisema chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ziruhusiwe kwa makundi maalumu.

Profesa Aboud alisema: “Pamoja na mapendekezo haya, Kamati Huru ya Kitaifa ya Ushauri wa Chanjo (NITAG) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), ziendelee kushirikishwa katika kutoa ushauri na kudhibiti chanjo hizo.”

Aliongeza: “Watu walio na hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona wapewe fursa ya kupatiwa chanjo hiyo.”

Rais Samia alitangaza kuunda kamati hiyo Aprili 6, mwaka huu ikiwa ni wiki chache baada ya kuapishwa, huku msisitizo mkubwa ukiwa katika kupambana na ugonjwa huo kwa njia za kisayansi.

Prof. Aboud alisema kamati hiyo ilifanyia kazi hadidu za rejea 12, zilizohusu maeneo mbalimbali ya tathmini ya mwenendo wa ugonjwa pamoja na afua za udhibiti ikiwamo chanjo hapa nchini, kikanda na kimataifa.

“Tangu kuingia kwa ugonjwa wa corona nchini Machi mwaka jana, Tanzania imekumbwa na mawimbi mawili makubwa. Na hivi sasa kutokana na mwenendo wa ugonjwa katika mataifa mengine duniani kuna tishio la kutokea kwa wimbi la tatu hapa nchini,” alisema Prof. Aboud.

Alibainisha kwamba baada ya uchambuzi uliofanywa na kamati, mapendekezo kwa serikali ni kuihuisha mipango ya dharura katika ngazi zote, kwa ajili ya kukabiliana na majanga ikiwamo ugonjwa wa corona.

Prof. Aboud alibainisha kwamba, kamati imependekeza serikali itoe taarifa juu ya uwapo wa ugonjwa huo, ichukue hatua madhubuti kuimarisha hatua zote za afua za kinga ili kuepusha wimbi la tatu la ugonjwa huo.

Alisema pendekezo lingine ni wataalamu wa afya watimize wajibu wao kitaalamu, kwa kuzingatia weledi, miiko na maadili katika kuelimisha, kukinga na kutibu ugonjwa huo nchini.

Lingine ni Tanzania ishiriki ipasavyo katika maamuzi na itekeleze maazimio ya kikanda na kimataifa, iliyoridhia katika Jumuiya za Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).

kuhusu matumizi ya chanjo, Prof. Aboud alisema kamati inashauri kwamba serikali kutumia vyombo vyake na kuendelea kuchukua hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo.

“Kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya corona nchini kwa kuanzia kiwe katika makundi muhimu, wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele wa utoaji wa huduma, mathalani watumishi sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji.

“Wazee na watu wazima kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50, wenye maradhi sugu, kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya figo,” alisema Prof. Aboud.

Pia Prof. Aboud alisema kamati pia inapendekeza chanjo hiyo ipewe kipaumbele kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wasafiri wanaokwenda nje ya nchi.

Alisema hivi sasa ufanyike uhamasishaji na maandalizi ya upokeaji, utunzaji, usafirishaji na utoaji wa chanjo nchini na wananchi kuwa huru kuamua kuchanja ama la.

“Serikali iratibu upatikanaji wa chanjo kwa watumishi wa taasisi za kimataifa walioko nchini, ijiunge na ‘COVAX Facility’ kwa kuwasilisha andiko la kupatiwa chanjo, kwa kutumia fursa inayotolewa na GAVI.”

“Serikali itumie fursa zilizopo wakati huu wa corona kuanza mchakato wa uanzishaji wa viwanda vya kutengeneza chanjo, iimarishe huduma za uchunguzi kwa kuijengea uwezo Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na maabara nyingine ili kupanua wigo wa upimaji wa ugonjwa,” alisema Prof. Aboud.

Prof. Aboud alisema kamati inapendekeza serikali kujenga uwezo wa ndani wa utambuzi wa virusi anuai vinavyosababisha ugonjwa wa corona na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Alisema serikali pia itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa corona kwa umma na WHO, ili wananchi wapate taarifa sahihi kutoka mamlaka za serikali na kuheshimu makubaliano na kanuni ambazo nchi iliridhia.

Mwenyekiti huyo alisema kamati inapendekeza kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kukamilisha mwongozo mpya wa matibabu ya ugonjwa huo.

“Serikali iendelee kuhakikisha kuwa matumizi ya tiba asili na tiba mbadala katika mfumo rasmi wa tiba za kisasa yanazingatia misingi ya kisayansi.

“Na serikali iendelee kutoa fursa na kuwawezesha wanasayansi kufanya utafiti kwa kufuata miiko, maadili na taratibu zilizowekwa ili kuimarisha kinga, tiba, uchunguzi wa ugonjwa wa corona na athari zake katika jamii nchini,” alisema Prof. Aboud.

Pia alisema kamati inapendekeza serikali kuendelea kuzingatia mazingira ya Kitanzania katika udhibiti wa corona katika kuamua kuweka au kutokuweka shuruti ya kujifungia na kuwa na ubunifu, ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta zinazochangia katika uchumi.