Bunge la Uingereza limefunguliwa tena rasmi baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita nchini England, Scotland na Wales. 

Kikao kipya cha bunge hilo kimefunguliwa rasmi na Malkia Elizabeth wa Pili, kulingana na utamaduni wa Uingereza. 

Malkia Elizabeth ameainisha miswaada kadhaa mipya itakayopendekezwa na serikali ya Waziri Mkuu Boris Johnson, ikiwemo wa sheria ya kuweka malengo ya kimazingira yanayofungamanisha kisheria, kukabiliana na shughuli za kiuadui kutoka mataifa mengine, kutoa mamlaka zaidi kwa serikali ya jimbo la Ireland Kaskazini na mageuzi ya mfumo wa uhamiaji.

Mtawala huyo wa Kifalme amethibitisha kuwa muswada tata wa sheria ya polisi, uhalifu, hukumu na mahakama, pia utawasilishwa tena bungeni. 

Akitangaza miswada hiyo, amesema kipaumbele cha serikali yake ni kulifufua taifa kutokana na madhara ya janga la virusi vya corona, na kulifanya kuwa imara zaidi, lenye afya na ustawi zaidi kuliko lilivyokuwa kabla. Hata hivyo Malkia hakuvaa barakoa wakati wa kikao hicho.