Mahakama ya Urusi imeahirisha kesi iliyopaswa kusikizwa kwa mara ya kwanza juu ya misimamo mikali ya mitandao ya kisiasa inayohusishwa na kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, mfungwa ambaye ni mkosoaji wa utawala wa Rais Vladimir Putin.

Wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea faraghani, upande wa mashtaka uliwasilisha nyaraka zaidi, hivyo kusababisha kesi kuahirishwa hadi Juni 9. 

Hayo ni kulingana na mawakili wanaowakilisha mitandao ya Navalny.Kesi hiyo inayolenga kuharamisha upinzani dhidi ya Rais Vladimir Putin, ni sehemu ya operesheni kabambe dhidi ya Navalny na wafuasi wake.

Kama sehemu ya jitihada hizo zinazojiri miezi michache tu kabla ya uchaguzi wa bunge, baraza la chini la bunge linatarajiwa kujadili hapo kesho mswada unaopiga marufuku wanachama wa mashirika yenye misimamo mikali kuchaguliwa kama wabunge.

Mwezi uliopita, waendesha mashtaka waliomba mtandao wa Navalny kwenye majimbo pamoja na Wakfu wake wa kupambana na ufisadi, kuorodheshwa kama mashirika yenye misimamo mikali, wakiyatuhumu kupanga maandamano makubwa yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi.