Korea Kaskazini imepuuza wazo la kufanya mazungumzo na Marekani siku moja baada ya utawala mjini Washington kusema uko tayari kwa majadiliano ya kidiplomasia kuhusu Pyongyang kuachana na mradi wake wa nyuklia. 

Wizara ya mambo ya kigeni ya Korea Kaskazini imesema haiko tayari kufanya mazungumzo na taifa linalotumia diplomasia "bandia" kuficha matendo yake ya uchokozi. 

Taifa hilo pia limemtahadharisha rais Joe Biden wa Marekani dhidi ya kuchukua kile imekitaja kuwa "msimamo uliopitwa na wakati" na kuonya kuwa Washington itapata madhara kwa kuichokoza Korea Kaskazini. 

Matamshi kutoka Pyongyang yanatolewa siku kadhaa tangu rais Biden alipoliambia bunge la Marekani kuwa utawala wake utatumia diplomasia pamoja na msimamo usioyumba kudhibiti malengo ya nyuklia ya Korea Kaskazini.