Georgina Misama- MAELEZO
Lugha ya Kiswahili imechaguliwa kuwa lugha rasmi kutumika katika mikutano yote itakayoendeshwa na Umoja wa Nchi za Afrika (AU).

Akiongea na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku Umoja wa Afrika, yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam  katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa nchi wanachama wa umoja huo zimekubaliana kutumia lugha ya Kiswahili kuendeshea mikutano yake yote.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika Kiswahili kama lugha halisi mojawapo ya kiafrika kimechaguliwa kuwa lugha rasmi  itakayotumika katika mikutano yote ya Umoja wa Afrika ambapo siku za nyuma Kiswahili kilikuwa kinatumika kama lugha ya kazi na katika ngazi ya Mikutano ya Maraisi tu. Jambo hili ni la kujivunia kwa sisi Watanzania na Afrika kwa ujumla”, amesema Mulamula.

Uamuzi wa kukichagua Kiswahili umeenda sambamba na utekelezaji wa kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hiyo kwa mwaka huu inayosema ‘Sanaa, Utamaduni na Urithi njia za Kuijenga Afrika tunayoitaka’.

Balozi Mulamula pia ameongelea upande wa  uchumi ambapo amesema mpaka sasa Afrika imepiga hatua kubwa kwani kuanzia Januari, mwaka huu   nchi za Afrika zilianza rasmi kufanya biashara chini ya Mkataba ulioanzisha Eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA). Mpaka sasa nchi 54 kati ya 55 za Afrika zimesaini mkataba huo ikiwemo Tanzania, aidha, nchi 37 zimeridhia mkataba huo na Tanzania ipo kwenye hatua za mwisho za kuridhia mkataba huo.

“Tanzania imeendelea kushiriki katika majadiliano ya kuondoleana ushuru wa bidhaa kwa nchi za Afrika, ambapo tayari imewasilisha mapendekezo yake kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Mchakato huo umekamilika kwa asilimia 75, ambapo utakapoanza kutekelezwa  bidhaa  zetu zitaweza kufika nchi yoyote  Afrika kwa urahisi zaidi”,amesema Balozi Mulamula.

Zoezi la makubaliano ya kuondoleana ushuru wa bidhaa litakapokamilika, hatua hiyo itasogeza zaidi Umoja wa Afrika kufikia lengo la kuimarisha uchumi wake, ambapo hili ni lengo lililopewa nguvu zaidi baada ya Afrika kujikomboa kisiasa. Malengo mengine ya Umoja wa Afrika ni pamoja na kudumisha umoja na mshikamano, Maendeleo ya Kisiasa, Kijamii na Kiuchumi na Afrika yenye Amani, Usalama na Utulivu.  

Balozi Mulamula ametoa rai kwa Watanzania, kujiandaa kutumia fursa za kibiashara kwa kuwekeza hasa katika viwanda na mazao ya biashara ili kupata bidhaa za kuuza katika nchi nyingine za Afrika. Tanzania itafaidika zaidi na mkataba wa kuondoleana ushuru wa bidhaa kwa nchi za Afrika kwa kuuza bidhaa zaidi ya kuuziwa.  

Aidha, Balozi Mulamula awewaomba waandishi wa habari, watumia nafasi hiyo kuitangaza kaulimbiu ya Umoja wa Afrika ya mwaka huu, ili kuwahamasisha Watanzania kuuelewa Umoja huo kwa undani ikiwa ni pamoja na historia yake, malengo yake, mwelekeo wake na namna ya kutumia fursa zinazotokana na Umoja huo lengo kubwa likiwa ni fursa za kibiashara.