Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kesi ya wafuasi  27 wa Chadema wakiwemo wabunge watatu waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko na kutotii amri halali katika geti la gereza la Segerea.

Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo na kuachiwa huru leo Jumatano Mei 5, 2021 na mahakama hiyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri hilo.

Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.

Hakimu Shaidi ameifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi kwa muda mrefu. Miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo ni mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na wabunge wenzake, Ester Bulaya na Esther Matiko.

Mbali na wabunge hao, washtakiwa wengine ni, aliyekuwa meya wa manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob;  Patrick Assenga; mfanyabiashara, Henry Kilewo na wengine 21.