Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma
Kamati Kuu ya Kitaifa ya Uratibu na Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ilikaa Mei 28, 2021 ambapo pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili na kuangazia namna bora ya kurahisisha ukamilishaji wa usimikaji wa Mfumo huo nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wenyeviti wa vitongoji na mitaa.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kazi nzuri imefanyika lakini hakukuwa na ushirikishaji yakinifu katika ngazi ya Serikali za vijiji/vitongoji na mitaa ili kurahisisha zoezi la ukusanyaji wa taarifa za makazi kutoka kwa wananchi.

Dkt. Chaula amekieleza kikao hicho matamanio yake ya kuona Usimikaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unamalizika nchini kwa kamati hiyo kuwa shirikishi, kutoa mrejesho kwa wakati na kuangalia namna bora ya kuunganisha mifumo inayotoa taarifa za makazi, barabara na vituo vya huduma za kijamii.

“Sisi wote tuliopo hapa tunajenga nyumba moja ambayo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tushirikiane kazi hii ifike mwisho”, alizungumza Dkt. Chaula

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mary Makondo amesema kuwa Wizara hiyo itashiriki kikamilifu kwa kutoa wataalam na vifaa vya kupima na kutambua maeneo yote nchini ili kurahisisha utekelezaji wa Mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kushirikiana ili hati za viwanja  zitakazokuwa zinatolewa siku zijazo ziwe zina anwani.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI Gerald Mweli amesema kuwa kazi kubwa inayotakiwa kufanyika ni kutoa elimu kwa umma na kuwatumia wenyeviti wa mitaa na vitongoji ambao ndio watakaorahisisha zoezi la usimikaji wa Mfumo huo kumalizika kwa wakati.

Aidha, kwa pamoja wajumbe wa kamati hiyo ambao ni kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tume ya TEHAMA (ICTC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na  Shirika la Posta Tanzania (TPC) walikubaliana kuunganisha nguvu kukamilisha usimikaji wa mfumo huo ambao kukamilika kwake kutarahisisha ufanyikaji wa mazoezi mengi ya kiserikali yanayotakiwa kumfikia kila mwananchi kama vile zoezi la sensa ya watu na makazi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari