Jumuiya ya ushirikiano wa mataifa 57 ya Kiislamu imekutana kwa dharura kujadili mapigano makali yanayoendelea baina ya Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas linalodhibiti ukanda wa Gaza. 

Waziri wa mambo ya nje wa mamlaka ya Palestina Riad al-Malki, amelaani mashambulizi ya Israel aliyoyaita ya uoga wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, akiongeza kuwa uhalifu unafanywa dhidi ya Palestina bila ya kuwepo na athari. 

Hata hivyo Mamlaka ya Palestina haina udhibiti dhidi ya kundi la Hamas na ukanda wa Gaza, ambako wapiganaji walichukua mamlaka mwaka 2007. 

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema Israel pekee ndio yenye kuwajibika na machafuko ya karibuni huko Jerusalem, Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo linakutana leo kulijadili suala hilo.