Israel na Hamas wamekanusha kwamba kuna mipango ya usitishwaji wa mapigano kati yao hivi karibuni wakati ambapo shinikizo linazidi huku makabiliano baina ya pande hizo yakiingia siku yake ya tisa. 

Izzat al-Rishak ambaye ni mwanachama wa ngazi ya juu wa Hamas kundi linautawala Ukanda wa Gaza amesema leo kuwa hakujakuwa na makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano na Israel. 

Televisheni moja ya Israel awali iliripoti kuhusiana na uwezekano wa kusitishwa mapigano kuanzia kesho saa tisa alfajiri. Kulingana na ripoti Israel nayo imekanusha uwezekano wa mapigano kusitishwa. 

Haya yanakuja wakati ambapo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema operesheni ya kurusha mabomu Gaza inalenga kuwanyamazisha Hamas.

"Kuna njia mbili tu za kukabiliana nao, unaweza kuwashinda na hilo linawezekana au unaweza kuwanyamazisha na sasa tunawakabili kwa nguvu lakini naweza kusema hatuondoi uwezekano wowote, tunatarajia tutarudisha utulivu kwa haraka. Tunafanya hivyo kwa makini ili tusiwaumize raia."

Taarifa za hivi punde zinaelezea kuwa rais wa Marekani Joe Biden amezungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kumueleza kuwa anatarajia kuona uhasama ukisitishwa. 

Hali kadhalika, jeshi la Isrel limesema limeyashambulia kwa mabomi maeneo kadhaa nchini Lebanon, kujibu mashambulizi ya maroketi yaliyorushwa kutoka maeneo hayo.