Mahakama ya kimataifa ya uhalifu - ICC yenye makao yake mjini The Hague imemhukumu kifungo cha miaka 25 jela, Dominic Ongwen, mwanajeshi mtoto aliyegeuka kamanda wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army, LRA la nchini Uganda. 

Ongwen alikutikana na hatia ya mashitaka 61 mwezi Februari, yakiwemo ya mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watu katika hali ya utumwa. 

Wakati wa uamuzi wao, majaji walisema Ongwen binafsi alitoa amri kwa wapiganaji wake kuwauwa watu wapatao 130 katika kambi za wakimbizi kati ya mwaka 2002 na 2005. 

Mkuu wa jopo la majaji hao Bertram Schmitt amesema wamekabiliana na hali isiyo ya kawaida, kwa sababu mtuhumiwa mbele yao alikuwa mhanga na mhalifu kwa wakati mmoja. 

Waendesha mashitaka walitaka apewe kifungo cha miaka 20, kwa hoja kwamba kutekwa kwake akiwa mwanafunzi na kuingizwa katika kundi kundi hilo la waasi, kunahalalisha kupunguziwa adhabu ambayo ingekuwa kifungo cha miaka 30 gerezani.