China Yaipatia Tanzania Msaada Wa Sh. Bilioni 35.37 Kwa Ajili Kutekeleza Miradi Ya Maendeleo
Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Serikali ya China imeipatia Tanzania msaada wa yuan za China milioni 100 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 35.37 utakaotumika kutekeleza miradi itakayokubaliwa ama kuridhiwa na pande zote mbili.
Mkataba wa makubaliano ya msaada huo umesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Wan Ke, kwa niaba ya Serikali ya China.
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa Mkataba huo, Bw. Tutuba alipendekeza msaada huo utumike kupanua ujenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kupandisha hadhi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwa Chuo Kikuu, kutekelea mradi wa uhifadhi wa Miamba katika eneo la Ngorongoro (Geopark), na miradi mingine itakayoafikiwa na Serikali zote mbili.
Aidha, aliishukuru China kwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu inayoipatia Tanzania kuanzia mwaka 2010 na kutumika kujenga miundombinu ya Reli, Elimu, Afya, Tehama, Nishati, Maji, Sekta ya Viwanda, Kilimo, Usalama, na Misaada ya Kitaalam, iliyofikia dola za Marekani bilioni 1.8 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 4.15.
“Nachukua fursa hii kukuhakikishia kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba miradi itakayotekelezwa kwa fedha za msaada huu inakamilika kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” aliongeza Bw. Tutuba
Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Wan Ke, alisema kuwa msaada huo ni matokeo ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Bw. Wang Yi, aliyoifanya mwezi Januari mwaka huu na ni mwendelezo wa ushirikiano mwema kati ya China na Tanzania uliodumu kwa zaidi ya miaka 57 sasa.
“Tangu wakati huo China imeisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA, Uwanja wa Michezo wa Benjamin Mkapa, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNCC), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam” alisema Mhe. Balozi Wan Ke.
Alibainisha miradi mingine iliyofadhiliwa na China kuwa ni upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro, Ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam ambapo miradi hiyo yote imekabidhiwa Serikali ya Tanzania.
“Vile vile tumewaleta madaktari wa kujitolea wapato 25 ambao wamekuwa wakijihusisha na utoaji wa tiba ya moyo na kupambana na malaria maeneo mbalimbali nchini na hivi sasa pia China imefadhili ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi mkoani Kagera ambacho ujenzi wake ukikamilika kitakuwa chuo kikubwa kuwahi kujengwa hapa nchini.
Aidha, Mhe. Wan Ke, alisema kuwa China imeipatia Tanzania msaada wenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.3 kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid 19 kwa ajili ya kununulia barakoa, vitakasa mikono, vifaa tiba na dawa na kwamba nchi yake imetia saini kushiriki kwenye mpango wa kuahirisha ulipaji wa madeni (DSSI) ili kuruhusu Serikali kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo mengine katika kupambana na maradhi hayo yanayoendelea kuitikisa dunia.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji wa China hapa nchini, Mhe. Balozi Wan Ke, alisema kuwa licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa Covd-19 na kuathiri uchumi wa nchi zote mbili, katika mwaka 2020, biashara na uwekezaji ulifikia dola milioni 4.58 sawa na ongezeko la asilimia 9.9.
“Uwekezaji wa mitaji wa China nchini Tanzania umefikia dola za Marekani milioni 159.71 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62.37 na kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu kiwango cha biashara kimekua kwa asilimia 59.71 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka uliopita 2020 huku bidhaa kubwa zinazoingia katika soko la China hivi sasa ni muhogo, mvinyo, na maharage ya soya” alisema Mhe. Ke.
Mhe. Balozi Wan Ke, alisema kuwa anaimani na uongozi wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kulinda uwekezaji ili kuwaongezea kujiamini zaidi na kwamba uamuzi huo unaungwa mkono na kampuni za China zilizowekeza hapa nchini na utawavuta wawekezaji wengi zaidi kutoka China kuja kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini.