Na Benny Mwaipaja, Arusha,
MAWAZIRI wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana Jijini Arusha katika mkutano wao wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi ambapo, pamoja na mambo mengine wamekubaliana kutoivunja Tume ya Kiswahili ya Jumuiya hiyo kutokana na umuhimu wa kukuza na kutumia lugha hiyo kwa mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Uamuzi huo umetokana na msimamo wa Tanzania na nchi za Kenya na Uganda ambazo zimekataa mapendekeo ya mtaalamu mshauri aliyependekeza kuvunjwa kwa tume hiyo na kupendekeza majukumu yake yasimamiwe na Idara ya Habari, Teknolojia, Utamaduni na Michezo iliyopo Sekretarieti ya Jumuiya kwa kushirikina na nchi wanachama ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Jumuiya hiyo.

Akichangia hoja kuhusu kuvunjwa kwa Kamisheni ya Kiswahili yenye Makao yake Makuu Zanzibar ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Jumuiya, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu lameck Nchemba (Mb) alisema kuwa hoja hiyo inalenga kudidimiza malengo na misingi liyopo ya kuiunganisha jumuiya na kwamba ni wakati wa kuienzi Kamisheni hiyo kwa kuifanyia mageuzi badala ya kufikiria kuivunja.

 “Tusiongelee suala la kiswahili kama lugha ya kufundishwa shuleni lakini tukione Kiswahili kama lugha inayotuunganisha kama wanajumuiya ya Afrika Mashariki” Alisisitiza Dkt. Nchemba.

Aidha katika kikao hicho, Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Fedha na Uchumi wamekubaliana na mapendekezo ya mshauri elekezi kuhusu kupunguza idadi ya wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka 9 kutoka kila nchi wanachama hadi kufikia wabunge 5 ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Jumuiya pamoja na kuongeza ufanisi.

Katika Mkutano huo nchi wanachama ziliwasilisha miongozo na kauli mbiu za bajeti za nchi wanachama kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbambali zilizowasilishwa kama vile taarifa za Kamati zinazoshughulikia masuala ya Fedha ikiwemo ile ya Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Nchi Wanachama pamoja na kufanya mashauriano ya awali ya Bajeti ya Mawaziri wa Fedha na masuala ya Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika, Mkutano huo umepokea Taarifa ya Utekelezezaji wa Maazimio mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza hilo la Kisekta pamoja na taarifa ya Utafiti wa kuboresha Mifumo na Miundo ya Uendeshaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kulingana na rasilimali zilizopo 

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Fedha wa Kenya, Mhe. Ukur Yatani Kanacho alitoa pole kwa niaba ya Mawaziri walioshiriki Mkutano huo kwa Ujumbe wa Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Aidha, alitoa pole kwa Nchi Wanachama kufuatia janga la ugonjwa wa Corona ambalo limeathiri uchumi wan chi nyingi na kuwataka wajumbe kuendelea kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Kadhalika kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Mhe. Dkt. Nchemba alipokea salamu za pole zilizotolewa na kusisitiza Nchi Wanachama kuendeleza umoja na mshikamano kama njia mojawapo ya kumuenzi Hayati Dkt. Magufuli.

Mkutano wa Mawaziri umepitisha kwa kauli moja kaulimbiu ya mwaka wa fedha 2021/2022 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki isemayo “Economic Recovery through Industralization and Inclusive Growth”.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo umewahusisha pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji Uchumi na Ajira Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga, Waziri, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali,   Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar, Bw. Mussa Haji Ali, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.

Mkutano huo ambao umeitishwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulitanguliwa na kikao cha Ngazi ya Wataalam kutoka Sekta za Fedha na Uchumi uliofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Mei 2021 na kufuatiwa na kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 6 Mei 2021.

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC zilizoshiriki mkutano huo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na nchi ya  Sudani Kusini haijahudhuria, ambapo nchi zilizoshiriki moja kwa moja kwenye mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Jijini Arusha ni Tanzania, Uganda na Burundi wakati walioshiriki kwa njia ya mtandao ni Kenya na Rwanda.

Mwisho