SALVATORY NTANDU
Mkazi wa kijiji cha Manyanda Masele Kuyela (52) anashikiliwa na jeshi  polisi mkaoni shinyanga kwa tuhuma za kumwozesha binti yake ambaye ni mwanafunzi wa kidato chapili (jina linahifadhiwa) kwa mahari ya ng’ombe sita na shilingi laki mbili.

Taarifa iliyotolewa na kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga,(ACP) Debora Magiligimba inasema kuwa Masele anashikiliwa pamoja na kaka wa bwana harusi ajulikanaye kwa jina la Pius Langa walipokuwa katika kikao cha kupanga mahari aprili 28 mwaka huu.

“Tulipata taarifa za kuozeshwa mwanafunzi huyo nyumbani kwao kijiji cha usanda ambako kikao cha kupanga mahari kilikuwa kinaendelea kufanyika maafisa wetu walipofika  eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wakiwa katika harakati za kupanga mahari,”alisema Magiligimba.

katika kikao hicho watuhumiwa hao walikubaliana mwanafunzi huyo kuolewa kwa mahari ya ng’ombe sita na fedha taslimu shilingi laki mbili ambayo ilitakiwa kulipwa mwezi mei mwaka huu ili shughuli za harusi ziweze kuendelea.

“Tunatarajia kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao baada ya upelelezi kukamilika na pia naomba nitoe wito kwa wananchi mkoani hapa kutoa taarifa zinazohusiana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa vyombo vya usalama ili viweze kutokomezwa,”alisema Magiligimba.

Mwisho.