Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Katika kuendeleza ushirikiano na Sekta binafsi, ambalo ni jukumu la kisheria la Serikali kuhamasisha sekta binafsi katika uzalishaji wa Mbegu Bora, Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda katika ziara yake Jijini Arusha, leo tarehe 30 Mei 2021 ametembelea moja ya kampuni binafsi ya uzalishaji wa Mbegu Bora za Kilimo nchini SEED.CO

Waziri Mkenda pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa Chimagu wamepata fursa ya kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Kampuni hiyo binafsi hasa katika suala zima la uchakataji na utunzaji wa Mbegu Bora unavyofanywa na kampuni hiyo kutoka hatua za awali Mbegu zinapotoka shambani, zinapopokelewa, kuchakatwa, kupimwa na kupakiwa tayari kwa kumfikia mkulima.

Katika ziara hiyo Waziri Mkenda amesema kuwa moja ya ajenda kuu ya Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha nchi inazalisha mbegu za kutosha za kilimo kupitia sekta binafsi kadhalika Mamlaka ya Mbegu ya Serikali (ASA) ili kufikia hatua ya kujitosheleza katika uzalishaji mbegu na kuanza kuuza nje ya nchi.

Amesema kuwa serikali inahimiza Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) pamoja na Taasisi zote zinazojihusisha na utafiti hususani wa mbegu kuhakikisha kuwa zinazendelea kufanya utafiti wa mbegu bora na zitakazo ongeza tija katika kilimo.

“Tunataka mtu aweze kuzalisha kiasi kikubwa zaidi kwa Hekari moja ili nguvu ya mkulima iwe inazaa matunda makubwa na vilevile itatusaidia sana kwenye masoko kwa sababu ukizalisha kwa wingi hata kama bei ya mazao imeshuka lakini kipato kinakuwa kikubwa” Amekaririwa Prof Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa pamoja na juhudi za serikali za kutumia taasisi ya utafiti (TARI) na mamlaka ya Mbegu (ASA) ambayo ina kazi ya kuchukua mbegu bora na kuzalisha kwa wingi ili kuzipeleka kwa mkulima lakini pia serikali inafanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ikiwemo kampuni ya mbegu ya SEED.CO

Prof Mkenda ameipongeza kampuni binafsi ya uzalishaji wa Mbegu Bora za Kilimo nchini SEED.CO kutokana na uzalishaji wa mbegu bora ambazo zimekuwa na matokeo mazuri kwa wakulima ambapo amewahakikishia hitaji lao kubwa la kukodi mashamba ya serikali kwa ajili ya uzalishaji mbegu bora linafanyiwa kazi kwa haraka iwezekanavyo.

“Lakini nimewaahidi endapo watajenga maabara kubwa ya kisasa kwa ajili ya shughuli za mbegu hapa Tanzania, nitajitahidi kuhakikisha kuwa wanapata mashamba makubwa angalau mawili kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu” Amesema Mkenda

Amewasihi kuongeza zaidi uzalishaji wa mbegu ikiwa ni pamoja na kuanzisha uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali badala ya Nafaka na Mbogamboga pekee, Kwa kufanya hivyo kutakuwa na uwezekano wa kuongeza mbegu bora na zenye tija kwa wakulima nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mbegu (TASTA) Ndg Bob Shuma amepongeza Serikali kwa kuamua kulichukulia kwa msisitizo swala la uzalishaji wa mbegu bora nchini ambapo ameeleza furaha yake na kumuhakikishia Waziri wa Kilimo kuwa umoja huo unaendelea na mkakati madhubuti katika uzalishaji wa mbegu bora na kwa wingi.

Hata hivyo amerejea msisitizo wa Waziri wa Kilimo kuyaomba mashirika mengine nchini na nje ya nchi kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya mbegu ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa karibu na serikali kupitia taasisi ya TARI na ASA ili kuongeza ufanisi katika sekta ya mbegu.