Zaidi ya watu 100 wameuwawa katika mashambulizi yaliyotokea jana kwenye kambi za jeshi nchini Somalia ambayo kundi la kigaidi la Al-Shabaab limethibitisha kuhusika. 

Magari mawili yaliyotegwa mabomu yaliripuka kwenye vituo viwili vya kijeshi kwenye wilaya ya Awdhegle na kijiji cha Bariire kwenye jimbo tete la Shabelle na kisha kufuatiwa na mashambulizi makali kutoka kwa wanamgambo wenye silaha waliovamia kambi za jeshi. 

Msemaji wa jeshi la Somalia amesema wamefanikiwa kuwadhibiti na kuwauwa wanamgambo 116 ikiwemo makamanda watatu wa kundi la Al Shabaab huku upande wa serikali umepoteza wanajeshi wanne. 

Kundi la Al Shabaab limedai kuhusika na shambulizi hilo kupitia kituo cha redio cha Andalus likisema wanajeshi 47 wa serikali wameuwawa.