Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho ameitaka Menejimenti ya Wizara kutoa ushirikiano kwa Naibu Mawaziri wa wizara ili kutimiza dhamira ya Serikali  ya kukamilisha miradi kwa wakati na ubora.

Akizungumza wakati wa kikao cha kumkaribisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mwita Mwaitara, Waziri Chamuriho amesisitiza umuhimu wa utoaji wa taarifa kwa wakati na kusisitiza uratibu mzuri wa utoaji wa taarifa hizo ili kuepuka mgongano.

“Mafanikio ya Wizara kwa sehemu kubwa yanategemewa na ushirikiano utakaooneshwa kuanzia kwenye usimamizi wa miradi mikubwa ya kimkakati na uratibu wa taarifa zinazotolewa kuanzia kwenye menejimenti na taasisi’ Amesema Waziri Chamuriho.

Waziri Chamuriho amesema Wizara imebeba miradi mikubwa ya nchi, ikiwemo reli, ndege, meli, vivuko, madaraja na barabara hivyo ni muhimu kwa Manaibu hao kujipanga kukagua miradi ya maendeleo kwa kushirikiana ili kubaini changamoto na kuzitafutia utatuzi wa haraka.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Godfrey Kasekenya amesema ushirikiano uliopo kati yake na Menejimenti umemfanya afanye kazi kwa weledi na kuifahamu sekta kwa haraka.

“Toka nimeteuliwa kuwa Naibu Waziri niseme ukweli nimepata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa menejimenti wakati wote nilipokuwa nikihitaji taarifa yoyote niliipata kwa wakati na kupewa maelezo ya kina” amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Naye Naibu Waziri Waitara ameomba kupata ushirikiano kwa kupewa taarifa za maendeleo ya miradi ya maendeleo kwa wakati ili kuweza kufanya kazi yenye matokeo chanya kwenye sekta mpya aliyoteuliwa.

Aidha, Katibu Mkuu- Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, amesema kuongezewa kiongozi kutaongeza chachu ya kuwajibika katika usimamizi na kuahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi wote  kwa wakati.

Mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu, 31 Machi, 2021 yameongeza Idadi ya Manaibu Waziri kutoka mmoja na kuwa wawili ili kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi.

Imetolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.