Waziri wa Tamisemi,  Ummy  Mwalimu amemsimamisha kazi mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sengerema,  Magesa Boniphace kupisha uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa leo Aprili 20, 2021 na kitengo cha mawasiliano serikalini imeeleza kuwa Waziri Ummy amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo kutoka kwa wananchi na viongozi mbalimbali akiwemo mbunge wa Sengerema (CCM), Hamisi Tabasamu.

Katika taarifa hiyo, tuhuma hizo zimeelekezwa kwa mkurugenzi na baadhi ya wakuu wa idara za halmashauri hiyo zinaonyesha wanafanya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo, na kuathiri utekelezaji wa miradi kwa kiwango kilichokusudiwa.

Kufuatia tuhuma hizo, Ummy amemuagiza katibu mkuu Tamisemi kuunda timu ya uchunguzi wa tuhuma hizo haraka.