WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemsimamisha kazi Ofisa anayesimamia Mnada wa Mifugo wa Upili ulioko Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora Bw. Juma Athuman kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mapato.

Mhe. Ndaki amechukua hatua hiyo juzi alipotembelea mnada huo ili kuangalia ufanisi wake ambapo alibaini kutokuwepo nyaraka za kumbukumbu ya mifugo inayoingia na kutoka katika mnada huo kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.

Alisema kukosekana kwa kumbukumbu hizo kumetoa mwanya wa upotevu wa mapato hivyo kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha, jambo hilo halikubaliki hata kidogo.

“Naagiza Uongozi wa Halmashauri kumwondoa kazini mara moja Ofisa Afya ya Mifugo Mohamed Kifamba na askari polisi wote waliokuwa wakisimamia mnada huo nao waondolewe mara moja, OCD shughulikia hilo” alisema Mhe. Ndaki.

Licha ya kusimamishwa kazi watuhumiwa hao Waziri Ndaki aliagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo za ubadhirifu wa mapato ya serikali kwa kipindi chote cha miaka 4 ili sheria ichukue mkondo wake.

“Kila siku ya mnada fedha nyingi zinakusanywa lakini hazionekani, zinaingia mifukoni mwa watu, hili halikubaliki na serikali haiwezi kufumbia macho vitendo vya namna hiyo kwa kuwa vinaikosesha mapato mengi sana,” aliongeza Waziri.

Aidha, alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kupeleka wataalamu wilayani humo ili kuchunguza mapato ya mnada huo yaliyopotea katika kipindi chote hicho ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa ikiwemo wahusika kulipa fedha hizo.

Pia waziri huyo alichukua hatua ya kumkaimisha msimamizi wa mnada huo Bw. Haidari Mwinyihija nafasi usimamizi wa mnada, wakati utaratibu wa kumpata Ofisa mwingine atakayesimamia mnada huo ukiendelea kufanyika.