WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuhusika na ulinzi wa watoto kwa kuweka mipango itakayoondoa mazingira yanayowafanya vijana balehe kuwa na tamaa ya vitu na kushawishika kujiingiza kwenye ngono katika umri mdogo.

”Suala la mimba za utotoni limekuwa mwiba kwa kipindi kirefu. Limekuwa likiwanyima wasichana wengi fursa ya kukamilisha malengo yao katika maisha. Hali hii haikubaliki lazima kila mmoja kwa nafasi yake aweke mikakati ya kuwawezesha watoto wa kike kumaliza masomo yao”.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Aprili 17, 2021) wakati wa uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe katika ukumbi wa Hoteli ya Morena, jijini Dodoma.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amesema programu za kuelimisha Vijana Balehe kuhusu madhara ya kuanza ngono mapema ziandaliwe ili washiriki kikamilifu katika masomo na masuala mengine ya maendeleo kwa kuwawezesha kupata taarifa sahihi.

Waziri Mkuu amesema takwimu za Elimu Msingi Tanzania (BEST – 2020) zimeonesha kuwa jumla ya watoto 1,135 katika shule za msingi na 5,340 katika shule za sekondari waliacha shule kwa sababu ya mimba hadi Desemba, 2020”.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha changamoto zinazolikabili kundi hilo zikiwemo za magonjwa ya kuambukizwa, upungufu wa taaluma sahihi za kujiajiri na kuajiriwa, matumizi ya dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wadau wote wa masuala ya afya na maendeleo ya vijana balehe nchini kubuni na kuandaa afua zilizofanyiwa utafiti zenye kuleta matokeo chanya katika kutokomeza mimba za utotoni.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Afya ihakikishe kuwa vijana balehe watakaothibitika kuwa na maambukizi ya VVU wanaunganishwa na huduma za tiba na matunzo ili wawe na afya njema itakayowawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Natoa rai kwa viongozi wenzangu, wataalamu na wadau wote mnaohusika na Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe nchini kuhakikisha kuwa ajenda hii inatekelezwa kwa vitendo ili hatimaye kutatua changamoto zinazowakabili vijana wetu ifikapo 2024/2025”.  Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema ajenda hiyo imeandaliwa kwa lengo la kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma rafiki za afya na kuondoa vikwazo vya maendeleo kwa vijana balehe nchini.

”Ajenda hiyo imejikita katika nguzo sita ambazo ni kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi, kutokomeza mimba za utotoni, kuzuia ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia, kuboresha  lishe, kuhakikisha watoto wa kike na kiume wanabaki shuleni na kuwajengea vijana balehe ujuzi na uwezo wa kuzifikia fursa mbalimbali za kiuchumi”.

Amesema katika kusaidia vijana balehe kupata fursa ya kujiendeleza kiujuzi na kiuchumi, ajenda hiyo inaelekeza kutanua wigo kwa programu ya ujuzi mwepesi (soft skills) kupitia Vyuo vya Elimu ya Ufundi (VETA) na vyuo vingine vya ufundi (Post Primary Training Colleges) kwa ajili ya vijana wanaomaliza shule za msingi ili kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

Waziri Dorothy amesema ajenda hiyo haina lengo la kuanzisha afua au programu mpya zinazokinzana na programu zilizopo katika sekta nyingine bali imelenga kuimarisha na kuboresha uratibu wa pamoja katika utekelezaji wa afua mbalimbali zinazohusu mahitaji mahsusi ya vijana wa rika balehe katika maeneo ya kimsingi yaliyoainishwa.